Seli shina ni nini?

Swahili

Seli shina ni nini?

Mwili wa binadamu una mamia ya seli (chembechembe hai) za aina tofauti zenye umuhimu kiafya.  Seli hizi zina jukumu la kuendesha mifumo mbalimbali ya miili yetu, kwa mfano, kuendesha mapigo ya moyo, kuwezesha fikra akilini, usafishaji wa damu kwenye figo, kutengeneza ngozi mpya, na kadhalika.  Kazi ya kipekee ya seli shina ni kuwa chimbuko la kuzalisha aina nyingine ya seli. Seli shina pia hufanya shughuli ya ugavi wa seli mpya mwilini.  Seli hizi zinapojigawanya huzidisha idadi ya seli shina nyingine au seli nyingine za kawaida.  Kwa mfano, seli shina za ngozi zinauwezo wa kuzalisha seli shina zingine zaidi za ngozi au kuzalisha seli tofauti zenye kazi maalumu kama kutengeneza melanin.

Kwanini seli shina ni muhimu kwa afya yako?

Tunapoumia ama kupata maradhi, seli zetu pia huumia au kufa.  Hali hii ikitokea, seli shina huanza kufanya kazi.  Seli shina zitaponya majeraha mwilini na pia kujaza nafasi ya seli zinazokufa mara kwa mara.  Kwa njia hii, seli shina zinatuweka katika hali ya afya nzuri na kudhibiti mwili kudhoofika mapema. Seli shina ni kama jeshi la matabibu wanaoonekana kwa hadubini pekee.

Kuna aina ngapi tofauti ya Seli Shina?

Seli shina huwa katika aina au mifumo mbalimbali.  Wanasayansi wanaamini kuwa kila kiungo mwilini kina seli shina zake maalumu.  Kwa mfano, damu hutengenezwa na seli shina za damu (hematopoietic stem cells).  Hata hivyo, seli shina huwepo kuanzia hatua za awali kabisa za uumbaji wa mwanadamu, na pale wanasayansi wanapootesha aina hizi za seli ndipo hufaamika kama “seli shina za kiinitete”. Sababu inayowafanya wanasayansi kuhusiana karibu na seli shina za kiinitete ni umuhimu wake katika kujenga kila kiungo cha mwilini wetu wakati wa uumbaji.  Hii humaanisha ya kuwa seli shina za kiinitete, tofauti na seli shina komavu, zina uwezo wa kubadilika na kuwa seli yoyote kati ya mamia ya seli za binadamu.  Kwa mfano, kwakuwa seli shina za damu zinauwezo wa kutengeneza seli za damu tu, seli shina za kiinitete zinauwezo wa kutengeneza seli za damu, mifupa, ubongo, na kadhalika.  Pamoja na hayo, seli shina za kiinitete zimepangwa kiasili kujenga seli shina nyingi na hata viungo, wakati seli shina komavu hazina uwezo huu.  Hii inamaanisha ya kwamba seli shina za kiinitete zina uwezo asilia mkubwa zaidi kurekebisha viungo majeruhi.  Seli shina za kiinitete huzalishwa kupitia mabaki ya viinitete vichanga kwenye vituo vya matibabu ya uzazi, matumizi ambayo ni muhimu la sivyo viinitete hivi hutupwa pasipo ya matumizi yake kwa ajili ya tafiti za tiba.

SSS au Seli Shina Shawishi ni nini?

Wanasayansi na matabibu duniani kote wamepata mategemeo mazuri kuhusu ujio wa  Seli Shina Shawishi (SSS).  Sababu kuu ni kuwa SSS zina sifa karibu zote za seli shina za kiinitete, ila hazizalishwi kutoka kwa viinitete.  Hivyo basi, hakuna pingamizi za kiimadili kuhusu matumizi ya SSS.  Zaidi ya haya, SSS hutengenezwa na seli ambazo siyo Seli Shina kutoka kwa mgonjwa mwenyewe, hivyo kuzipa SSS uwezo wa kurudishiwa kwa mgonjwa bila hatari ya kushambuliwa na mfumo wa kinga wa mwili. Jambo hili ni la umuhimu katika tiba yoyote ya upandikizwaji wa Seli Shina.

Kuna mategemeo yapi kuhusiana na Seli Shina na jinsi ambavyo zitaleta mapinduzi katika tiba?

Jukumu la seli shina ni kubadilisha seli zenye majeraha, ugonjwa au seli zilizokufa. Wanasayansi wamepata wazo la kutumia seli shina katika tiba kwa ajili ya wagonjwa wa maradhi ya aina mbalimbali.  Wazo lao kuu ni kuwapa wagonjwa seli shina au seli komavu zilizozalishwa na seli shina. Kwa namna hii wanatumia nguvu asilia ya Seli Shina kutibu na kumrudisha mgonjwa katika hali ya afya tena.  Kwa mfano, kama mgonjwa amepata shinikizo la moyo, tiba itakayotumika ni kupandikiza seli shina kwa mgonjwa ili kutibu majeraha kwenye moyo.  Kwa kawaida idadi ya seli shina tulizonazo mwilini zina uwezo mdogo kurekebisha majeraha.  Tukirudi kwenye mfano wa shambulizi wa moyo, seli shina za moyo hazina uwezo wa kutosha wa kuponya majeraha yanayotokana na shinikizo la damu, lakini pale mamilioni ya seli shina za moyo zitakapopandikiwa uwezo wa tiba huongezeka maradufu.  Hivyo basi kwa kuwapandikiza wagonjwa kutumia seli shina tunaongeza uwezo wa mwili kuponya zaidi ya uwezo mdogo wa kiasilia.  Changamoto chache bado zipo kabla matibabu ya seli shina kuwa tiba ya kidesturi, kwa mfano changamoto za usalama kwasababu ya uwezo wa baadhi ya seli shina kutenegeneza uvimbe wa saratani, na pia changamoto ya mashambulio ya mfumo wa kinga wa mwili.  Hata hivyo seli shina huenda zikaleta mageuzi makubwa kwenye matibabu, na pengine baada ya muongo au miongo miwili wengi wetu, pengine hata sisi wenyewe, tutakuwa tunafahamu mtu aliyetibiwa kwa kupandikizwa na seli shina.  Seli shina zimeshikilia ahadi ya kuwa na uwezo wa kutibu magonjwa mengi yanayomsibu binadamu kama saratani, magonjwa ya moyo, ugonjwa wa Parkinson, Uzulufu mwingi, kiharusi, ugonjwa wa Huntington, majeraha ya uti wa mgongo na magonjwa mengine mengi.

Ni tiba gani ya Seli Shina inayopatikana kwa sasa, na kwanini matabibu wengi wanashauri uzingatie tahadhari aina hii ya tiba iwe chaguo la mwisho?

Hivi sasa, kuna tiba chache zinazotumia seli shina zilizo na ufanisi pamoja na uthibitisho wa usalama.  Mfano bora zaidi ni upandikizaji wa uhogo wa mfupa.  Hata hivyo, tiba mbalimbali za seli shina hutangazwa na kunadiwa dunia kote.  Mara nyingi tiba hizi hutangazwa zaidi kwenye vyombo vya habari, hasa pale ambapo watu maarufu kama wanamichezo wanapopata tiba za aina hizi.  Kiujumla, wanasayansi na matabibu kwenye fani ya seli shina hutoa tahadhari kuhusu tiba hizi kwasababu bado haijafahamika iwapo aina hii ya tiba ni salama na ni fanisi.  Wagonjwa wengi wamefariki kutokana na tiba ya aina hii.  Pamoja na kuwa ni jambo la busara kuzingatia njia zote unapopatwa na maradhi au magonjwa yasiyotibika, tunashauri uzingatie tiba hii kama chaguo la mwisho na iwe baada ya kushauriwa na mganga wako.

Translators: Daniel Maeda, George Rugarabamu, Steven Nyabero, Vincent Rwehumbiza, and Edwin Swai

Subscribe to Our Newsletter

Subscribe to Our Newsletter

Be the first to know about the latest developments in stem cell and regenerative medicine research.

5 thoughts on “Seli shina ni nini?”

  1. Nasikia Ugonjwa wa Cirhosis(Ugonjwa wa ini) unasabisha kujaa maji tumboni sababu ya makovu katika ini kuziba mishipa katika ini .Je hakuna dawa ya kuondoa makovu hayo na kuruhusu seli mpya kuzalishwa?

  2. Hongera kwenu…. kumbe mambo haya yanaonekana magu ila kwa kiswahili ni rahisi ivi…. safi sana kwa kazi nzuri👏🏾👏🏾👏🏾

  3. Safi sana. Kwa juhudi hizo naamini siku moja Kiswahili inaweza kuwa lugha ya kufundishia Sayansi katika ngazi zote za elimu hapa Tanzania na kwingineko.

Leave a Reply